
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemwondoa Luhaga Joelson Mpina, mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT–Wazalendo kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kufuatia pingamizi liliowasilishwa na Hamza Saidi Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya uteuzi wa Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.
Kufuatia kikao chake kilichofanyika tarehe 15 Septemba, 2025, INEC imefanya uamuzi wa kumwondoa Mpina, hivyo kuwa pingamizi pekee lililokubaliwa kati ya mapingamizi manne (04) yaliyowasilishwa mbele yake, ambapo pingamizi matatu (03) yamekataliwa.
Tume ilipokea mapingamizi matatu tarehe 13 Septemba, 2025, dhidi ya uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT – Wazalendo na tarehe 14 Septemba, 2025, ikapokea pingamizi moja (01) dhidi ya uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
INEC imekataa mapingamizi yaliyowasilishwa na Ndugu Almas Hassan Kisabya mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha NRA dhidi ya Luhaga, na pingamizi la Ndugu Almas Hassan Kisabya mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha NRA dhidi ya uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.
Pingamizi liliowekwa na Ndugu Kunje Ngomale Mwilu, mgombea kiti cha Rais kupitia chama cha AAFP dhidi ya Ndugu Luhaga Joelson Mpina, mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo limekataliwa pia huku Tume ikikataa na kutupilia mbali pingamizi liliowekwa na Luhaga Mpina dhidi ya uteuzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).