Jumatano , 17th Jul , 2019

Baada ya kumaliza muda wake wa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Augustino Mrema, amesema yupo tayari kuendelea, endapo Rais Magufuli atamteua tena.

Augustine Mrema

Mrema ameyasema hayo leo Julai 17, 2019 kupitia kipindi cha East Africa Drive cha East Africa Radio, ambapo ameeleza mpango wake wa kuwatoa wafunga takribani 5000.
 
''Pamoja na kipindi changu kuisha lakini nipo tayari kuendelea endapo Rais Magufuli ataniteua tena na lengo ni kutimiza ndoto yangu ya kutoa wafungwa zaidi ya 5000'', amesema.

Aidha Mwanasiasa huyo nguli ameongeza kuwa Katika kipindi chake cha miaka mitatu kilichomalizika Julai 16, 2019, amefanikiwa kuwatoa wafungwa zaidi ya 600.

Kwa upande mwingine Mrema ameiomba Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia kwa Mawaziri wake ambao ni Mh. Kangi Lugola na Naibu wake Hamad Masauni, iharakishe michakato ya kuwatoa wafungwa wanaopendekezwa na Bodi ya Parole ili kupunguza msongamano wa wafungwa kwenye Magereza nchini.

Mrema aliyeteuliwa na Rais John Magufuli, kuongoza bodi hiyo Julai 16, 2016, hivyo jana Julai 16, 2019, alitimiza kipindi cha miaka  mitatu cha kuongoza bodi hiyo.