Jumatano , 12th Aug , 2020

Mbunge aliyemaliza muda wake kupitia CHADEMA Mchungaji Peter Msigwa, amesema kuwa anaamini kuwa kuna figisu nyingi zitafanywa kuelekea Uchaguzi Mkuu, lakini anapenda uchaguzi wa mwaka huu uwe huru na wa haki.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 12, 2020, mara baada ya kuchukua fomu ya uteuzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili agombee nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo kwa mara nyingine tena kwenye ofisi ya Msimamizi wa uchaguzi huo Jimbo la Iringa.

"Tumemwandikia barua Mkurugenzi kwamba kuna baadhi ya wasimamizi hatuna imani nao kabisa kwa kuwa wameonesha ukada wa CCM, tungetaka watu wengi, tunaamini kwamba figisu zitafanywa lakini sisi tungependa uchaguzi ulio huru na wenye haki kwa sababu tunaipenda nchi yetu" amesema Mchungaji Msigwa. 

Zoezi hilo la uchukuaji na urejeshaji fomu kwa ngazi ya Ubunge na Udiwani, kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi limefunguliwa leo na litahitimishwa Agosti 25, 2020.