Jumatano , 12th Dec , 2018

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya CUF, Abdallah Mtolea amesema licha ya kujiuzulu kwenye nafasi yake bado ana mahusiano mazuri na waliokuwa wabunge wenzake wa upinzani na kusisitiza kuwa mahusiano hayo yatazidi kuendelea.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya CUF, Abdallah Mtolea.

Mtolea ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv iliyotaka kufahamu juu ya namna ambavyo amejipanga kuhakikisha anawania tena nafasi ya Ubunge kwenye jimbo hilo baada ya kuhama chama.

Mtolea amedai siasa haina udaui na kwamba wabunge wote ni watu ambao amekuwa akishirikiana nao kila siku.

"Mimi sina uadui na Mbunge yeyotete, kwa kifupi wabunge wa vyama vyote ni marafiki zangu, kuhusu kama wanahofu kwamba ukaribu wangu nitakuwa nikiwashawishi wabunge wengine wahame mimi siwezi kuwasemea," amesema Mtolea.

"Kuhusu suala la nani atakuwa mpinzani wangu kwenye uchaguzi wa marudio bado sijajua maana mimi bado sijapitishwa kugombea tena na uteuzi utafanyika Disemba 20," ameongeza.

Novemba 15 mwaka huu, Abdallah Mtolea alitangaza kujivua nafasi yake ya Ubunge na kwa kile alichokidai kuchoshwa na mgogoro uliokuwa ukiendelea kwenye Chama cha Wananchi CUF ambapo baadaye altangaza kujiunga Chama Cha Mapinduzi CCM.