Jumamosi , 13th Apr , 2019

Mtoto Idrissa Ally (13), mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Pronces Gate jijini Dar es Salaam, amerejea nyumbani kwa wazazi wake baada ya kutekwa na watu wasiojulikana Septemba 26, 2018.

Idrissa alirejea nyumbani jana April 12 majira ya jioni, huku wazazi wake ambao walikuwa tayari wamekata tamaa, walimpokea na kujawa na furaha iliyotoweka kwa kipindi kirefu.

Tangu Septemba 2018 siku alipotekwa hadi April 2019 (jana) alipopatikana, Idrissa amefikisha siku 198 za kuishi mbali na familia yake huku akishindwa kuendelea na masomo.

Baba mzazi wa Idrissa amesema jana jioni, mama mzazi wa mtoto huyo, Leila Kombe, alipokea ujumbe kutoka katika namba asiyoifahamu na kuelezwa kuhusu kutafutwa na mtoto wake. Hata hivyo, hakuamini kwa kuwa ameshapokea ujumbe wa aina hiyo mara nyingi, kumtaka mume wake apige namba hiyo.

"Nilimpigia akaniambia yupo Ubungo na kwamba mtoto wake aliomba ampigie lakini ameshaondoka akielekea nyumbani kwao Tegeta”, amesema Idd ambaye ni baba wa kijana huyo.

Amesema hakuamini lakini kama miujiza saa moja jioni aliona pikipiki ikiingia nyumbani kwake ikiwa imempakia kijana wake, “bado siamini kama amerudi nyumbani, tumekuwa kwenye giza nene kwa muda mrefu", amesema  Baba wa mtoto huyo.

Mzazi wa mtoto huyo amesema mwanaye amebadilika na kuwa mrefu, huku akiwa na nywele nyingi, “inaonekana hakuwahi kunyoa tangu alipotekwa”.

Akiendelea kuhojiwa ni kwa namna gani ameweza kuachiwa alikotekwa, Idrissa amesema kuwa kuna kijana mmoja alimsaidia kumtorosha, alimpatia nauli akimtaka aende Dar es Salaam kwa wazazi wake.

Idrissa alitekwa Septemba 26,2018 saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo alichukuliwa na dereva mwanaume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST. Dereva huyo alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo na kumuingiza mlango wa nyuma wa gari na kuondoka naye.