
Athuman Mwasomora (11), mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mapambano wilayani Rungwe Mkoani Mbeya, amefariki dunia akidaiwa kujinyonga kwa kamba ya begi kwenye fremu ya mlango ndani ya chumba alichokuwa akilala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amebainisha hayo jana Septemba 7, 2025 na kuongeza kuwa, tukio hilo lilitokea Septemba 2, 2025 majira ya saa 4.30 asubuhi katika Kijiji cha Lulasi, Kata ya Mpombo Halmashauri ya Busokelo Wilaya ya Rungwe.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, lilianza uchunguzi wa kisayansi kwa kushirikiana na daktari wa Kituo cha Afya Ruangwa Halmashauri ya Busokelo Wilaya ya Rungwe huku kamanda Kuzaga akitoa taarifa hiyo kufuatia video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha Ester Pangapanga (28), mama mzazi wa marehemu akidai mtoto ameuawa.
Kufuatia tukio hilo mama mlezi wa mtoto huyo Mariam Mwakasusa (38) anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.