Jumamosi , 2nd Apr , 2016

WAZIRI wa Habari,sanaa,utamaduni na michezo Nape Nnauye amesema Muswada wa Sheria ya huduma za vyombo vya habari uko mbioni kurejeshwa tena bungeni hivi karibuni.

Akizungumza na wadau wa wizara yake kutoka Mikoa ya Mbeya na Songwe kwenye mkutano uliofanyika jijini Mbeya,Nnauye amesema muswada huo ambao awali ulikumbana na vizingiti vingi yakiwemo malalamiko ya wamiliki wa vyombo vya habari sasa uko katika hatua za mwisho kurejeshwa bungeni.

Waziri Nape Amesema tayari muswada huo umefumuliwa na kuleta usawa kutokana na malalamiko ya awali na ana imani wabunge watakubaliana nao na kuupitisha.

Amewaahidi wanahabari kuwa na imani na muswada huo akisema pamoja na kufumuliwa kwa muswada huo bado umelinda maslahi yao hivyo siku ukipitishwa itakuwa neema kwao.

Hata hivyo amesema kupitishwa kwa muswada huo kunaweza kuwa mwiba kwa baadhi ya wamiliki wa vyuo vya taaluma ya habari nchini hususani vinavyotoa taaluma hiyo pasipo kuzingatia ubora unaostahili.

Awali akiwasilisha taarifa ya Chama Cha Waandishi wa habari mkoa wa Mbeya(MBPC),Katibu wa chama hicho Emanuel Lengwa amemuomba waziri huyo kubainisha ni wapi mchakato wa Muswada huo umefikia huku akisema kutomalizika kwa mchakato huo kunaendelea kusababisha wanahabari kuminywa stahiki zao na wamiliki wa vyombo vya habari.

Lengwa pia amebainisha uwepo wa utitiri wa vyuo vinavyojitangaza kutoa taaluma ya habari lakini ukweeli ni kuwa taaluma inayotolewa haina mchango kwa tasnia hiyo zaidi ya kuidhalilisha kwa kuzalisha wahitimu wasio na uwezo wa kufanya kazi.