Jumatano , 17th Sep , 2025

Anashutumiwa kwa kufyatua risasi ya bunduki moja kutoka juu ya paa iliyopenya shingo ya Kirk Jumatano iliyopita kwenye kampasi ya Chuo Kikuu cha Utah Valley huko Orem, kama maili 40 (kilomita 65) kusini mwa Salt Lake City.

Waendesha mashtaka wa Utah wameapa jana Jumanne Septemba 16 kutafuta hukumu ya kifo kwa mshtakiwa muuaji wa mwanaharakati mhafidhina Charlie Kirk na kufichua maelezo mapya ya kesi yao, ikiwa ni pamoja na ujumbe mfupi wa maandishi ambapo alidaiwa kukiri kwa siri kumpiga risasi mtu huyo.

Kulingana na nakala za jumbe zilizohusishwa na mshukiwa katika nyaraka za mahakama zilizowasilishwa na waendesha mashtaka , Tyler Robinson, 22, alimwambia mwenzake na mpenzi wake alichoshwa na chuki ya bwana Kirk, alipoulizwa kwa nini alifanya mauaji hayo, aidha, DNA iliyopatikana kwenye kifyatulia risasi cha silaha inayodaiwa kuwa ya mauaji ilihusishwa na Robinson, waendesha mashtaka walisema.

Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Utah Jeffrey Gray ilimshtaki Robinson kwa makosa saba ya jinai siku ya Jumanne, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kuchochewa, kuzuia haki kwa kutoa ushahidi na ulaghai wa shahidi kwa kumtaka mwenzake kufuta maandishi ya hatia. Baadhi ya wanasiasa, akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump, wametoa wito wa hukumu ya kifo katika kesi hiyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Gray alisema amefanya uamuzi wa kutafuta hukumu ya kifo kulingana na ushahidi uliopo na mazingira na asili ya tukio hilo.

Robinson alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza jana  Jumanne alasiri kupitia video kutoka jela, akiwa hajanyoa nywele na akiwa amevalia vazi maalumu la kuzuia kujiua. Hakujieleza lakini alionekana kusikiliza kwa makini huku hakimu akisoma mashtaka na kumfahamisha kuwa anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo. Mshtakiwa alizungumza mara moja tu, alipotakiwa kutaja jina lake.

Robinson kwa kuwa hawezi kumudu mawakili wa kisheria, Jaji wa Wilaya ya Nne ya Utah Tony Graf alisema atateua wakili wa utetezi kabla ya kusikilizwa kwa kesi ijayo, iliyopangwa Septemba 29. Wakati huo huo, amewekwa  katika Jela ya Kaunti ya Washington, ambapo, kulingana na msemaji wa sheriff, amewekwa chini ya itifaki ya saa maalum ambayo inajumuisha usimamizi ulioongezeka.

Kirk, 31, mwanzilishi mwenza wa vuguvugu la wanafunzi wa kihafidhina la Turning Point USA na mshirika mkuu wa Trump, alikuwa akizungumza katika hafla iliyohudhuriwa na watu 3,000 alipouawa kwa kupigwa risasi. Watetezi wa haki za kiraia kwa muda mrefu wamemkosoa Kirk kwa matamshi ya kudharau makundi mbalimbali yaliyotengwa, ikiwa ni pamoja na Weusi, Waislamu, wahamiaji, wanawake na watu waliobadili jinsia, na kwa kukumbatia madai yasiyothibitishwa ya Trump ya kuibiwa kwa uchaguzi wa 2020.

Wafuasi wa Kirk wanamtaja kama mtetezi shupavu wa maadili ya kihafidhina na bingwa wa mijadala ya umma ambaye aliwachochea wapiga kura vijana kupitia Turning Point, na kuchagiza mvuto wa vuguvugu la MAGA kwa wapiga kura wa Gen Z.