Alhamisi , 2nd Mei , 2024

Kijana mmoja anayefahamika kama Boaz Sanga ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza, amefariki baada ya kuzama wakati akijaribu kuogelea kwenye ziwa Viktoria.

Mwili wa Boaz Sanga, Mwanafunzi wa CHuo cha SAUTI Mwanza baada ya kupatikana Pembezoni wa Ziwa Viktoria

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mwanza Kamila Laban, amesema kijana huyo alienda na wenzake ziwani katika maeneo ya Sweya na baada ya muda aliamua kuanza kuogelea pasipo kujua urefu wa kina cha maji na hivyo kupelekea kuzama.

SACF Kamila amesema baada ya Zimamoto kufika eneo la tukio zoezi la kumtafuta liliendelea hadi jana usiku bila mafanikio na leo Mei 02, 2024 wamefanikiwa kuupata mwili wake pembezoni mwa mawe ziwani hapo.

Kwa upande wake mlezi wa wanafunzi chuoni hapo Fr. Japhet Njaule amesema kijana huyo na vijana wenzie wawili walienda ziwani kwa ajili ya kupiga picha, ndipo kijana huyo alizama na kupotelea ndani ya maji.

Hata hivyo Jeshi la zimamoto limetoa rai kwa watumiaji wa ziwa Viktoria kuwa makini katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.