Jumanne , 27th Feb , 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, ACP Salum Morcase amkamate Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya wilaya ya Serengeti, Saad Mutunzi Ishabailu kwa kosa la kuhamisha shilingi milioni 213,748,085 kwa awamu nne kwa njia ya uhamisho

Kushoto ni Mweka hazina na kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

wa ndani kwa kushirikiana na watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.
 
Ametoa agizo hilo leo Jumanne, Februari 27, 2024, wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Serengeti kwenye kikao kilichofanyika katika Halmashauri hiyo, mkoani Mara. 

"Mkamate huyo bwana sasa hivi aende polisi akafunguliwe mashtaka, huyu ni wa kupeleka mahakamani moja kwa moja. DPP aelezwe afungue jalada la mashtaka, wale wenzake tumewapeleka mahakamani tayari sababu tulibaini walihusika na wizi kama huu kwenye Manispaa ya Kigoma mwaka jana," amesema Waziri Mkuu

Amesema Juni 21, mwaka jana Bw. Ishabailu alianza kufanya matumizi ya hizo fedha kwa kushirikiana na mfanyabiashara wa hapa Mugumu, Bw. Daudi Matinde Chacha kupitia kwenye akaunti zake za NMB na CRDB kwa kupitia miamala minne ya sh. milioni 76.3, sh. milioni 57.7, sh. milioni 47 na sh.milioni 32.5.

Amesema alipoulizwa na timu ya uchunguzi Bw. Matinde alikiri kuwa haidai fedha yoyote Halmashauri ya Serengeti isipokuwa Mweka Hazina huyo aliomba apitishie fedha zake kwenye akaunti zake kwa sababu zinahitajika haraka kwa matumizi ya ofisi.  “Aliambiwa atoe shilingi milioni 189 akamkabidhi zote Bw. Ishabailu na zilizobakia (sh. milioni 24) akaambiwa abaki nazo,” amesema Waziri Mkuu.