Jumanne , 2nd Mar , 2021

Mzee mmoja aliyefahamika kwa majina ya Joseph Rutabana mwenye umri wa miaka 77 mkazi wa kijiji cha Butairuka amepoteza maisha, baada ya kutumbukia katika kisima cha maji, kilichochimbwa katika eneo la Kanisa Katoliki Parokia ya Maruku, katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera.

Kaimu Mkuu wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika wilaya ya Bukoba, Mkaguzi Msaidizi Abrahman Ngaugia, amesema kuwa walipata taarifa za kwenda kufanya maokozi saa kumi mchana, na kwamba walipofika eneo la tukio askari wa jeshi hilo Sajenti Karata Ramadhan ndiye aliyeingia katika shimo hilo na kufanikiwa kuutoa mwili wa mzee huyo kwa kushirikiana na askari wenzake.

Kwa upande wao baadhi ya ndugu, majirani na viongozi wa eneo hilo wamesema kuwa siku tatu kabla ya tukio, mzee huyo alionekana kama amechanganyikiwa na kuwa wakati akiondoka nyumbani aliaga kwamba anakwenda kuoga.