
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imesema kuwa itaendelea kushirikiana na wizara za kisekta katika kuhakikisha kijiji cha Msomera kinaendelea kuwa cha mfano kwa kukiwekea miundombinu yote wezeshi kwa ajili ya wananchi wanaohamia.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Abdul-razaq Badru alipotembea kijiji hicho cha Msomera kilichopo wilayani Handeni Mkoani Tanga kujionea uendelezaji wa eneo hilo ambalo linatumika kwa ajili ya kuwamishia wananchi tarafa ya Ngorongoro wanaojiandikisha kuhama kwa hiari.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya kuna kazi kubwa ambayo serikali imefanya, tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha kijiji hiki kinakuwa bora ili wananchi waliohamia na wale watakaohamia waweze kuishi hapa kwa furaha,” Kamishna Badru amesema.
Naye, Mkuu wa wilaya ya Handeni mhe. Nyamwese amesema kuwa kazi mbalimbali za uboreshaji wa miundo mbinu katika kijiji hicho zinaendelea ikiwa ni pamoja na ulinzi wa Nyumba ambazo zimeshakamilishwa kujengwa.
Kijiji cha Msomera kimekuwa ni cha mfano kutokana na serikali ya awamu ya sita kuamua kuweka miundombinu yote ya msingi ili wananchi wanaoishi eneo la Ngorongoro waweze kuhamia kupisha shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo.