Jumanne , 1st Sep , 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuanza kusikiliza rufaa zilizokatwa na wagombea wa ngazi za Ubunge na Udiwani kutoka majimboni ambapo hadi sasa tayari imepokea rufaa 557 ambazo inaanza kuzishughulikia mara moja kuanzia leo.

Mwenyekiti wa NEC Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa NEC Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage ambapo amefafanua kuwa hatua hiyo inajiri baada ya kukamilisha mchakato wa Uteuzi wa majina ya wagombea wa  vyama mbalimbali vya siasa kwa nafasi ya Urais hii leo.

"Leo tumeanza  kuzisikiliza Rufaa zilizowasilishwa na wagombea waliokata  kutoka majimbo mara baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya awali, baada ya kusikiliza tutatoa maamuzi kulingana na sheria na taratibu zilizopo", amesema Jaji Kaijage.

Wakati huo huo Tume imetoa wito kwa makundi mbalimbali kuendelea kuheshimu sheria za uchaguzi zilizowekwa ili kuhakikisha kila raia mwenye haki ya kupiga kura wanatimiza wajibu wao kikatiba.