Ijumaa , 11th Jan , 2019

Katibu wa Itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM amepinga suala la Mbunge wa Bunda Mjini kutambuliwa na kupewa sifa kwamba aliwatetea wafanyakazi juu ya mafao kwa kipinga hadharani kikokotoo kipya na badala yake itambuliwe serikali ya CCM chini ya Rais Magufuli.

Pichani, Kushoto ni Rais wa Tanzania, John Magufuli, (kulia) ni Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole katikati.

Akizungumza na www.eatv.tv, Polepole amesema kwamba aliyesimama na jambo la kikokotoo tangu mwanzo ni serikali ya CCM na aliyehitimisha jambo hilo ni Rais Magufuli mwenyewe.

Ameongeza kwamba Rais Magufuli baada ya kusikiliza maoni ya wawakilishi na baadhi ya viongozi wa wafanyakazi akaamua kufanya maamuzi ambapo pia aliweka utaratibu na utaratibu huo umeshaanza kufanya kazi.

"Ni dhambi kuchukua sifa ambayo si yakwako. Siyo kweli kwamba ni yeye, aliyesimama na jambo hili, tangu mwanzo ni serikali ya CCM na aliyehitimisha jambo hilo ni Rais Magufuli mwenyewe. Maoni na mitazo ilikuwa mingi, ni haki ya kila mtanzania kila mmoja ana uhuru wa maoni. CCM inaheshimu uhuru hatutashangaa kila mtu akiweka maoni hadharani.

Mwezi Novemba mwaka uliopita, Spika wa bunge alimsifu Mbunge wa Bunda Mjini (CHADEMA), Ester Bulaya, ambaye pia ni Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), aliyeibua suala kutumika kwa kanuni mpya kwenye mafao ya wastaafu.

Bulaya aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kikokotoo hicho kipya kilichotungwa na serikali ni kitanzi kwa wastaafu kwa kuwa hawatanufaika na fedha zao ambazo wamezitolea jasho kwa miaka mingi.

Baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi, Rais Magufuli alipokutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), vyama shiriki, watendaji wakuu wa mifuko ya Hifadhi ya jamii ya PSSSF na NSSF na Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) Desemba 28, aliagiza kikokotoo kilichokuwa kikitumika awali kieendelee katika kipindi cha mpito mpaka mwaka 2023.