Nilimpeleka binti yangu kununua sidiria - Master

Jumatano , 13th Jun , 2018

Producer mkongwe wa muziki wa bongo fleva nchini Tanzania Master Jay, amefunguka na kuwaonya wababa wote wenye mabinti wa kike kuacha tabia ya kuwatenga watoto wao pindi wanapokuwa wamevunja ungo kwani kwa kufanya hivyo kuna uwezokano wa kumuharibu kisaikolojia.

Master Jay ametoa kauli hiyo leo Juni 13 wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha DADAZ kinachorushwa kila Jumatano kutokea EATV zikiwa zimebakia siku chache kuadhimisha siku ya baba Kimataifa na kusema imekuwa kawaida kwa wababa kupenda watoto wao wa kike lakini wanakuja kuwatenga wanapokuwa wamevunja ungo.

"Wababa wengi wa Tanzania kwa jinsi nilivyowaona wanawapenda watoto wa kike lakini wanapata shida pale mabinti zao wanapovunja ungo kwa mara ya kwanza na kupelekea wababa wengi kushindwa kuendelea kudeal na mtoto wa kike", amesema Master Jay.

Aidha, Master Jay amedai kwa upande wake haikuweza kumpa shida kubwa sana pindi binti yake alipovunja ungo kwa kuwa anaamini mtoto wa kike mapenzi yake yote yapo kwa wazazi wa kiume nasio mama.

"Mimi nilimpeleka mwanangu alipovunja ungo kununua sidiria. Nawaomba wababa muache kuwatenga watoto wa kike wanapokuwa wamevunja ungo", amesisitiza Master Jay.

Kwa upande mwingine, Master Jay amedai watoto wengi wa kike nchini wamekuwa wanaharibika kiakili kutokana na kutopata mapenzi ya baba yake mzazi kama alivyokuwa mdogo huku akiwasisitizia wababa wenzake kutokimbia majukumu yao kwa mabinti zao.