
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shana ameeleza kazi anayotarajia kuifanya baada ya kustaafu kazi ya upolisi, ni kuwa anatamani kuwa mchungaji wa kuhubiri injili na si kuingia kwenye siasa.
Kamanda Shana ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya kudaiwa na baadhi ya watumiaji wa mitandano ya kijamii, kuwa amekuwa akijihusisha na masuala ya siasa wakati yeye akiwa afisa mkubwa wa Jeshi la Polisi.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum #EATV/EARadioDigital Kamanda Shana amesema "mimi nikistaafu kazi pekee ninayotaka kuifanya si siasa bali kuwa mchungaji wa Injili tena nitakuwa Muhibiri wa Kimataifa, mimi nampenda Mungu, kwa hiyo nitahubiri upendo na umoja."
"Kuhusiana na kujutia juu ya kauli zangu ninazozitoa kuhusiana na Chama Cha Mapinduzi mimi siwezi kujutia, kwa sababu huwa naitwa kwa ajili ya kueleza nilichofanya kupitia ilani ya chama tawala" amesema Kamanda Shana.
Hivi karibuni akizungumzia akiwajibu baadhi ya watu mtandaoni ambao walihoji juu ya kuonekana kwenye mikutano ya CCM na kutumia baadhi ya kauli za CCM Kamanda Shana aliwataka watu hao wakaangilie Katiba ya CCM.