Ijumaa , 11th Jul , 2014

Waziri wa maliasili na utalii nchini Tanzania Lazaro Nyalandu, ametangaza kuivunja idara ya wanyamapori na kuunda mamlaka ya wanyamapori, kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake kiasi cha kusababisha matukio ya ujangili na uwindaji haramu.

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, mhe. Lazaro Nyalandu.

Waziri Nyalandu ametangaza hayo leo jijini Dar es Salaam sambamba na kutangaza kufuta leseni za uwindaji na uendeshaji wa vitalu vyote vilivyotolewa kwa kampuni ya Green Miles Safaris ambayo hivi karibuni waziri kivuli wa maliasili na utalii Mchungaji Peter Msigwa alianika kile alichokiita ukiukwaji mkubwa wa sheria ya wanyamapori.

Kwa mujibu wa Waziri Nyalandu, majukumu yote yaliyokuwa chini ya idara ya wanyamapori yatakuwa chini ya mamlaka ya wanyamapori itakayoundwa hivi karibuni, mamlaka aliyosema itakuwa na mamlaka kamili ya kiuendeshaji na kusimamiwa moja kwa moja na wananchi.

Jumpili iliyopita, Waziri kivuli wa maliasili na utalii Mchungaji Peter Msigwa alionesha kwa waandishi wa habari mkanda wa video na kuanika kile alichookiita kuwa ni uozo na ukiukwaji mkubwa wa sheria ya wanyama pori unafanywa kupitia vitalu vya uwindaji.

Mchungaji Msigwa alifichua namna makampuni yaliyopewa leseni ya uwindaji ikiwemo ya Green miles Safaris Ltd, ilivyovunja sheria ya wanyamapori kwa kuwauwa wanyama wadogo, kufanya ukatili wakati wa kuwakamata na hata kukiuka sheria za kimataifa ambazo Tanzania kama nchi imeziridhia.

Aidha, Mchungaji Msigwa alimtaka waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu kuwawajibisha watendaji wote katika idara ya wanyamapori sambamba na kuchukua hatua kali dhidi ya kampuni ya Green Miles Safaris ikiwa pamoja na kuifutia kampuni hiyo leseni ya uwindaji.
…........................................