Jumatano , 8th Oct , 2025

Hati  iliyosajiliwa ya mwaka 2025 na kupewa namba 24514 baada ya kupokelewa kwa maombi hayo  itasikilizwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi, siku ya kesho  Alhamis Oktoba 9.

Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es salaam imepanga kusikiliza maombi ya Wakili Peter Kibatala juu ya madai ya kutekwa kwa Mwanasiasa Humphrey Polepole siku ya kesho  Oktoba 9, 2025.

Maombi ya Wakili Kibatala yaliwasilishwa mahakamani jana, Oktoba 7, 2025 akiiomba mahakama itoe amri ya Polepole kufikishwa mahakamani ama mamlaka husika ziseme yupo wapi kufuatia tukio la kutekwa kwa Balozi huyo wa zamani nchini Cuba ambaye taarifa zake zilisambaa katika mitandao ya kijamii siku ya Jumatatu Oktoba 6,2025.

Hati  iliyosajiliwa ya mwaka 2025 na kupewa namba 24514 baada ya kupokelewa kwa maombi hayo  itasikilizwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi, siku ya kesho  Alhamis Oktoba 9.

Wakili Kibatala ameiomba Mahakama iingilie kati mara moja akidai kuwa Polepole alitekwa nyara alfajiri ya Jumatatu, Oktoba 6, 2025, kutoka katika makazi yake yaliyoko eneo la Ununio, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na watu wasiojulikana wanaoshukiwa kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi la Tanzania.

Katika hati hiyo ya dharura Wakili Kibatala ameieleza Mahakama kuwa Polepole hajawahi kushtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika Mahakama yoyote, na kwamba kwa sasa inaaminika anashikiliwa katika eneo lisilojulikana na maafisa wa Jeshi la Polisi.

Maombi hayo yamewasilishwa dhidi ya wajibu Maombi watano, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RPC).