Alhamisi , 28th Jan , 2021

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge, amesema operesheni iliyofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama katika kata ya Mabwepande, Januari 24 na 25, mwaka huu imewakamata watuhumiwa 314 wa uhamihaji haramu na baada ya mahojiano watu 84 pekee ndiyo waliobainika ni wahamiaji haramu.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge

RC Kunenge amebainisha kuwa katika uchunguzi uliofanyika, baadhi ya watuhumiwa walibainika kuwa na viashiria vya kujihusisha na uhalifu wa wizi, unyang'anyi, uporaji wa ardhi na kuuza kwa utapeli pamoja na kuzuia wamiliki halali wa ardhi kuingia katika maeneo yao jambo linalozua migogoro ya ardhi.

RC Kunenge ameongeza kuwa kati ya watuhumiwa hao 84, 79 wanatokea nchini Burundi, wawili wanatokea nchini Malawi,  DRC Congo wawili  na mmoja kutoka nchini Msumbiji, na kubainisha kwamba watuhumiwa hao wote watafikishwa mahakamani kwa kosa la kuishi nchini kinyume na sheria.

Aidha RC Kunenge, amesema watuhumiwa wengine 33 bado wanaendelea kuchunguzwa uraia wao huku wengine 197 waliobaki waliachiliwa baada ya kubainika kutokuwa na dosari katika uraia wao.