Maria Basso, aliyeuawa Septemba 14 na panya road
Tarifa hiyo imetolewa leo Septemba 18, 2022 na Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo Jumanne Muliro, ambapo tukio hilo lilitokea baada ya Polisi kupata taarifa fiche kutoka kwa wananchi, juu ya uwepo wa kundi la wahalifu wapatao 9 waliokuwa tayari katika gari aina ya Toyota wakitokea Mabibo kuelekea Goba kufanya tukio kubwa la uvamizi wa nyumba kadhaa za kupora mali.
Kamanda Muliro ameongeza kuwa, baada ya kufika eneo la Makongo waliliona gari hilo na walipotaka kuwakamata wahalifu walishuka na kuanza kuwatishia mapanga Polisi kwa maana ya kukaidi kukamatwa kwao licha ya Polisi kujihami kwa kufyatua risasi hewani na ndipo waliposhambuliwa na kujeruhiwa na baada ya kupelekwa hospitali walifariki kwa bahati mbaya.
Aidha uchunguzi umebaini kuwa watu wawili kati ya wahalifu hao ni viongozi wa kundi hilo na wametambuliwa kwa majina ya Salum Juma Mkwama, maarufu Babu Salum, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 27-30, mkazi wa Mbagala na Khalifan Khalifa mkazi wa Buguruni, waliwahi kushtakiwa kwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2021.
"Upelelezi wa awali pia umebaini kuwa watuhumiwa hao waliotambuliwa majina yao, wanadaiwa kushiriki katika tukio la mauaji la tarehe 14 Septemba 2022 Usiku lililotokea huko Kawe Malingo pamoja na matukio mengine ya kuvunja nyumba usiku, kujeruhi kwa mapanga na kupora mali yaliyotokea siku za hivi karibuni," imeeleza taarifa ya Kamanda