Jumatano , 13th Jan , 2016

Uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia 6.9 katika kipindi cha robo tatu ya mwaka mmoja uliopita huku pato la taifa kati ya Januari na Septemba mwaka jana likifikia fedha za Tanzania shilingi trilioni 70.7.

Uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia 6.9 katika kipindi cha robo tatu ya mwaka mmoja uliopita huku pato la taifa kati ya Januari na Septemba mwaka jana likifikia fedha za Tanzania shilingi trilioni 70.7.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt Albina Chuwa amesema hayo leo wakati akitoa ripoti ya pato la taifa katika robo ya tatu inayoanzia Julai hadi Septemba mwaka jana, ambapo katika kipindi hicho pato la taifa limekuwa kwa kasi ya asilimia 6.3.

Aidha, Dkt Chuwa amesema kuwa katika kipindi hicho shughuli za kiuchumi zimekuwa zikiimarika ambapo mauzo ya nje ya Tanzania yameongezeka kwa wastani wa asilimia 3.3 huku kiwango cha uagizaji bidhaa kikiwa kimeshuka kwa asilimia 0.58.

Wakati huo huo imeelezwa kuwa mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita haukuwa wa kuridhisha.

Moja ya sababu zilizochangia hali hiyo imetajwa kuwa ni kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni pamoja na ongezeko la bidhaa bandia sokoni.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda nchini—CTI, Bw. Hussein Kamote, amesema hayo leo na kwamba kushuka kwa thamani kumesababisha wenye viwanda washindwe kuagiza malighafi kwa ajili ya uzalishaji viwandani.

Aidha, kuhusu kuwepo kwa bidhaa bandia na zisizokidhi viwango; Kamote amesema bidhaa hizo zimekuwa zikiua soko la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani, kwani licha ya kuwa chini ya kiwango, bidhaa hizo zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya kutupa kwani waagizaji wamekuwa wakitumia gharama ndogo tofauti na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.