Jumamosi , 15th Dec , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amewataka wasanii kutumia mitandao ya Kijamii kuhamasisha masuala ya Utalii wa nchi ili waweze kuitangaza Tanzania kupitia wafuasi wao wa mitandao ya kijamii ambao wanapatikana nchi mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kulia), na Amber Rutty.

Akizungumza Jijini Dar es salaam, mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, pamoja na Waziri Maliasili na Utalii Dkt Hamis Kigwangalla, Makonda amewataka wasanii wapewe nafasi ya kutangaza utalii huo.

Makonda amesema "niwaombe wananchi wa Dar es salaam tutumie fursa hii kutangaza utalii wetu, niwaombe wasanii wenye wafuasi mitandaoni watangaze utalii wetu hapa nchini ili dunia ifahamu kuliko kusambaza picha za Amber Rutty ambazo zinaleta joto kali na laana".

"Tunatamani Dar es salaam isiwe sehemu ya kupita bali iwe sehemu ya watu kukaa, kwa sababu tuna maeneo ya utalii, ikiwemo ghorofa la kwanza kujengwa Tanzania liko Dar es salaam."

"Nimuombe Waziri Kigwangala barabara ya kutoka Airport iwekwe mabango ya utalii, ili kutangaza nchi yetu na utajiri tuliokua nao," Ameongeza Makonda.