Jumamosi , 18th Mei , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Benki ya CRDB uzidi kuzingatia misingi ya utawala bora na kuongeza juhudi katika utoaji wa huduma, ili benki hiyo iendelee kuwa mfano wa mafanikio kwa taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na wazalendo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya 5 inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeendelea kuimarisha misingi ya utawala bora ili kuleta matokeo chanya, hivyo ni vema kwa uongozi wa benki hiyo ukaizingatia.

Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali kunakuwepo na uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu, usawa, kuzingatia taratibu za kisheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Viongozi wakuu wa kitaifa.”

Serikali imeendelea kusisitiza uwazi katika kuendesha shughuli za umma na makampuni yanayomilikiwa na wananchi bila usiri na kificho, lengo ni kuwapa wananchi uwezo wakupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria.” amesema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wa jinsia zote na makundi yote wanahusishwa katika kupanga nakufanya maamuzi ya mambo yanayowahusu ili kuwawezesha kujiletea maendeleo.