Polisi Pwani wamsaka anayeuza nyama za wizi 

Alhamisi , 13th Mei , 2021

Jeshi la Polisi mkoani Pwani, linamsaka mfanyabiashara wa nyama ambaye jina lake limehifadhiwa kwa tuhuma za kuchinja mifugo ya wizi na kuuza kwenye mabucha yake kitu ambacho amesema si salama kwa walaji.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa, amesema kuwa jeshi hilo lilipokea taarifa za kupotea kwa mifugo ambayo ni ng'ombe 25 na mbuzi 31, mali ya Rajabu Maulid, yenye thamani ya zaidi ya shilingi milion 50 hali iliyopelekea jeshi lake kuanza msako wa kuwatafuta wahusika wa tukio hilo.

Aidha, Kamanda Nyigesa amesema msako wa Polisi umebaini mabucha saba katika maeneo ya picha ya Ndege, Kwamatiasi, Loliondo, Kilivya Kwakomba na bucha zote hizo zinadaiwa kumilikiwa na mfanyabiashara huyo.

Kamanda Nyigesa ameongeza kuwa vitu vilivyokamatwa katika msako huo ni kilo 235 za nyama iliyokamatwa na kuteketezwa na wataalamu wa Idara ya mifugo, pamoa na ng'ombe wanne mali ya Rajabu Maulid ambao aliwatambua huku vitu vingine vilivyokamatwa ni ngozi za ng' ombe nane na mbuzi 24 ambapo zote ni mali za Rajabu.