Jumapili , 18th Sep , 2022

Jeshi la Polisi nchini limeongezewa nguvu na makampuni binafsi ya ulinzi ili kuzuia uhalifu wa panya road ndani ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo makampuni hayo yameahidi kutoa magari 8, pikipiki 3, askari na mafuta yenye thamani ya Tsh 350,000, ili kusaidia katika doria mbalimbali.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini CP Awadhi Juma Haji.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini CP Awadhi Juma Haji, na kusema kwamba miongoni mwa waliokamatwa kufuatia na uhalifu wa panya road ni wale waliowahi kufungwa kutokana na makosa madogo madogo ya uhalifu.

"Huu uhalifu ulioko mbele yetu ni wa kawaida kabisa na si ule wa kupangwa ni wahalifu kama walivyo wengine kutokana na changamoto za maisha kimaisha na ndiyo hao wanatusumbua, wahalifu wengi wamekamatwa na ufuatiliaji unaendelea," amesema CP Haji

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Jami CP Faustine Shilogile amesema Makampuni binafsi ni wadau wa ulinzi namba moja hivyo ni vyema kushirikiana na Jeshi la Polisi na kuongeza kuwa malengo ya kikao yamefikiwa kwa kiasi kikubwa na kushughulikia baadhi ya changamoto zilizobainishwa na viongozi wa makampuni hayo.