Alhamisi , 17th Nov , 2022

Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamefariki dunia kutokana na kupigwa risasi na polisi usiku wa kuamkia jana, baada ya kutokea majibizano ya risasi baina ya kundi la watu watano na askari, katika Kijiji cha Muganza, Kata Mursagamba wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera William Mwampaghale

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera William Mwampaghale, amesema kuwa kuuawa kwa watu hao kumetokana na oparesheni maalumu inayofanywa na jeshi hilo katika maeneo mbalimbali ya mkoa hasa mipakani, inayolenga kudhibiti uhalifu wa kutumia silaha iliyoanza mwezi Septemba mwaka huu.

Kamanda Mwampaghale amesema kuwa wakati wakiendelea na oparesheni hiyo Novemba 15, 2022 walipata taarifa fiche kutoka kwa raia wema kuwa kuna kundi la watu wanajiandaa kufanya uhalifu kwa kutumia silaha, na kwamba ilipotimu saa 04:30 usiku waliweka mtego katika barabara itokayo Bugarama kwenda Muganza na kufanikiwa kuwaona watu hao.

"Waliamrishwa na polisi kusimama lakini walikataa na kuanza kupiga risasi, kwa kuwa kulikuwa na giza na ni usiku, polisi walijibu na kuwajeruhi watu watatu wenye jinsia ya kiume wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 35 ambao hawajatambuliwa kwa majina, na watu hao walifariki wakati wakipelekwa hospitali ya Nyamiaga, huku wengine wawili wakikimbia" amesema RPC Kagera .

Kwa mujibu wa Kamanda huyo miili ya watu hao watatu imehifadhiwa katika hospitali ya Nyamiaga wilaya ya Ngara ikisubiri utambuzi na kwamba katika eneo la tukio ilipatikana bunduki moja aina ya AK 47 isiyokuwa na namba, ikiwa na magazine moja yenye risasi 12.