Alhamisi , 21st Oct , 2021

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo amesema ni wakati sasa wa kujenga jamii ya kidijitali kwa kuhakikisha huduma mbalimbali za kiserikali zinapatika kwa pamoja kupitia dirisha la huduma za pamoja.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Macrice Mbodo

Mbodo ameyasema hayo leo wakati akitoa mchango wake kwenye Kongamano la Tano la Mkutano Mkuu wa TEHAMA 2021, ambapo amesema kwa kufanya hivyo itarahisisha huduma zote kuwa pamoja hata kama ni kuzipata mtandaoni.

''Ili kujenga jamii ya kidijitali kwa upande wa serikali ni muhimu sasa kuhakikisha tunakuwa na huduma za pamoja kwenye dirisha moja ili mwananchi aweze kufanya malipo ya huduma mbalimbali sehemu moja, kodi zote, Uhamiaji, Polisi, Elimu na huduma nyingine,'' ameeleza Macrice Mbodo, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania. 

Washiriki mbalimbali wakifuatilia wachangia mada

Kwa upande mwingine Mbodo amesema, ''Dirisha lenye huduma za pamoja litasaidia kuondoa changamoto iliyopo sasa ambayo humlazimu mwananchi kutafuta huduma au kufanya malipo ya serikali kwenye madirisha tofauti tofauti, inatakiwa akifika sehemu moja anamaliza mahitaji yake yote ya kiserikali,''.

Mkutano Mkuu wa TEHAMA 2021 unaendelea katika ukumbi wa Simba ndani ya Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa Arusha na leo ni siku ya pili na utamalizika kesho Ijumaa Oktoba 21, 2021 kwa kutolewa tuzo za ICT Awards 2021.