Jumamosi , 7th Sep , 2019

Jimbo la Mikumi kupitia Mbunge Joseph Haule maarufu kama Prof Jay imethibitisha kufariki kwa Mweka Hazina wao wa Baraza La Wanawake wa CHADEMA Jimbo la Mikumi, Tishi Charles ambaye amefariki leo Septemba 7, 2019.

Mbunge wa Mikumi Joseph Haule na Marehemu Tishi Charles ambaye alikuwa mweka hazina wa BAWACHA Mikumi.

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, Prof Jay ameeleza kwamba Tishi Charles alikuwa akisumbuliwa na Saratani na alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Ocean Road akipatiwa matibabu.

"Mimi kwa sasa nipo Mikumi tupo tunafanya Misa ya kumuombea Baba yetu leo ametimiza mwaka mmoja tangu atutoke, hivyo hii asubuhi ndiyo nimepokea simu kuwa mwenzetu Tishi Charles amefariki," amesema.

"Kwa sasa bado taratibu za mazishi hatujajua tunafanyaje ila sio muda mrefu tutakaa sisi kama CHADEMA kwaajili ya kupanga nini kinafuata, ikiwemo kusafirisha mwili kutoka Dar es salaam kuja Mikumi" ameongeza.

Akieleza mchango wa Tishi Charles, Prof Jay anasema watamkumbuka kwa uchapakazi wake, kushirikiana na wanawake, kutetea haki za watoto na zaidi alikuwa mshiriki mzuri katika miradi ya maendeleo.

"Alikuwa ni mtu ambaye hajali Chama, alikuwa anashiriki sehemu yoyote kwa manufaa ya jamii, kapambana sana kusimamia haki za akina Mama kama unajua Mama ni nguzo kubwa ya maendeleo," aliongeza zaidi.