Jumatano , 27th Apr , 2016

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, amewatahadharisha kuwawajibisha maafisa elimu wa shule za msingi watakaoshindwa kusimamia elimu na kusababisha wanafunzi wamalize shule za msingi bila kujua kusoma na kuandika.

Waziri wa Elimu,Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako

Prof. Ndalichako amesema hayo Mjini Iringa katika mafunzo ya wakaguzi na wadhibiti wa ubora wa elimu mashuleni kutoka wilaya 31 kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Prof. Ndalichako amesema kuwa ni aibu kwa wanafunzi waliosoma miaka saba darasani hawajui kusoma na kuandika wakati Wakaguzi na Wasimamizi wa Elimu wapo katika maeneo husika na kuwataka wajitathimini kama wanatekeleza wajibu wao ipasavyo.

Waziri huyo pia amewataka wadhibiti hao wa elimu kufanya ukaguzi wa vitabu na vifaa vya kufundishia vikiwa na ubora unaokubalika huku akiahidi kuzingatia mahitaji ya walemavu katika shule za serikali.

Kwa upande wao walimu pamoja na wadhibiti hao wa elimu wameiomba serikali kushughulikia madai yao na kuboresha mazingira ya kufanyika kazi ikiwemo pamoja na fungu la kutosha na kuendeshea ukaguzi wa elimu.

Sauti ya Waziri wa Elimu,Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof.Joyce Ndalichako akitoa Onyo kwa wasimamizi wa walimu