Jumatano , 6th Aug , 2014

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali nchini Tanzania imepanga kufanya msako wa kuondoa sokoni na kuwakamata wafanyabiashara wa vilainishi visivyokidhi viwango vya kutumika kulainisha vipouri vya mitambo na magari.

Mkemia Mkuu wa Serikali nchini Tanzania, Profesa Samwel Manyele.

Mkemia mkuu wa serikali Profesa Samwel Manyele amesema hayo leo jijini Dar es Salaan na kufafanua kuwa msako huo unatokana na ofisi yake kubaini kuwepo sokoni kwa kiwango kikubwa cha shehena ya vilainishi hivyo visivyokidhi viwango.

Kwa mujibu wa Profesa Manyele, tayari kampuni mbili zimebainika kuhusika na kuingiza vilainishi hivyo ambapo ofisi yake imetoa muda wa siku sitini kwa waingizaji hao kuondoa sokoni shehena isiyofaa na kwamba baada ya hapo msaki utaendeshwa wa kuondoa vilainishi feki na wahusika wake kukamatwa.

Profesa Manyele amesema vilainishi visivyokidhi viwango vimekuwa vikiharibu magari na mitambo, sambamba na kuisababishia serikali hasara kwa kuikosesha malipo halali ambayo yangetokana na vilainishi halali ambavyo vingeingizwa nchini na kulipiwa ushuru.

Mkemia mkuu huyo wa serikali amewataka waagizaji na wauzaji wote wa vilainishi pamoja na kemikali nyingine, kuzingatia taratibu na sheria za uingizwaji wa kemikali hizo, ikiwa ni pamoja na kuwa na nyaraka muhimu kutoka kwa mamlaka za serikali, ili kuonyesha kuwa bidhaa wanazoingiza zimekidhi viwango na kufuata taratibu.

Aidha, Profesa Manyele amewataka wananchi kuzingatia ubora wa bidhaa za vilainishi wanavyokwenda kununua kipindi hiki, wakati ofisi yake ikiendelea na uchunguzi wa jinsi vilainishi hivyo vilivyoingizwa nchini na namna ya kuhakikisha vinaondoka katika soko.