
Bw Odinga alikuwa amesema muungano huo ulikuwa umeapa kutowasilisha kesi mahakamani wakati huu, wameona ni heri kufanya hivyo ili kuficha uovu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu.
Kiongozi huyo ameishutumu Tume Huru ya Uchaguzi Kenya akisema imekuwa ikitangaza matokeo ya uchaguzi bila kutoa Fomu 34A za kuonyesha matokeo yalivyokuwa katika vituo vya kupigia kura.
Aidha amesema mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa hata kumfanya Kenyatta kupata ushindi
"Tumeamua kwenda mahakamani kufichua jinsi uongozi wa kompyuta ulivyofanikishwa. Hawa ni viongozi wa kompyuta. Kompyuta ndiyo iliwataga, kompyuta iliwaangulia, kompyuta iliwatoa vifaranga vya kompyuta. NASA inaamini kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki" " amesema Odinga akiwahutubia wanahabari mtaa wa Lavington, Nairobi.
Hata hivyo Kiongozi huyo wa upinzani amesema udukuzi huo una uhusiano na kuuawa kwa meneja wa teknolojia katika tume hiyo Chris Msando ambaye aliuawa wiki moja kabla ya uchaguzi.
Pamoja na hayo Odinga amewashutumu waangalizi wa uchaguzi ambao walisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.
Pamoja na hayo Kiongozi huyo amesema kuwa upinzani uliwahi kufika mahakamani kupinga matokeo mwaka 2013 lakini hawakutendewa haki, na kusema mahakama ilidai Uhuru Kenyatta alishinda kwa asilimia mia huku wao wakipoteza asilimia zote
"Mahakama inaweza kutumia hii kama nafasi ya pili ya kujitakasa, au inaweza kuamua kuharibu mambo kabisa,"
Matokeo yaliyotangazwa na tume huru huko nchini Kenya IEBC yameonyesha Rais Uhuru Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku mpinzani wake Raila Odinga akipata kura 6,762,224.