Jumanne , 18th Dec , 2018

Rais wa Chama Cha Wanasheria nchini TLS, Fatma Karume amefafanua juu ya kauli ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma aliyoitoa hivi karibuni juu ya kuwa Mawakili wengi nchini wanaohitimu hawajui kujieleza vizuri kwa kingereza na kusema kauli hiyo haikulenga kuwadhalilisha mawakili.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Rais wa Chama Cha Wanasheria nchini TLS, Fatma Karume.

Kwa mujibu wa Fatuma Karume ambaye ni maarufu kwa jina la 'Shangazi', Jaji Mkuu ndiye mtu wa mwisho anayekaa na mawakili nchini baada ya kumaliza masomo ya elimu ya juu na kuwafanyia mahojiano ili kufahamu uwezo wa mawakili kujieleza.

Akizungumza na www.eatv.tv, Fatuma Karume amesema, "si kweli kuwa kauli ya Jaji Mkuu ni kuwadhalilisha wanasheria, bali amesema ili kuhamasisha wazidi kusoma lugha ya kingereza na wazidi kupata uwezo mkubwa zaidi kwenye kingereza, lengo kubwa lilikuwa kujenga na si kubomoa."

"Wanasema amedhalilisha, kwani kusema ukweli ni kudhalilisha?, yule pale amezungumza na kila wakili na kama ameona vile maana yake ni kweli kwa sababu kabla hajawaapisha huwa anazungumza na kila mmoja wao, yeye ndiyo anajua uwezo wao," ameongeza Fatuma Karume.

Akizungumza juzi wakati akiwaapisha mawakili wa kujitegemea 909, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma alieleza kuwa kati yao mawakili 800 hawawezi kujieleza kwa lugha ya kingereza.