Jumatatu , 13th Aug , 2018

Rais Dkt. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya wakuu wa wilaya pamoja na kuteua wakurugenzi wapya 41 wa halmashauri za wilaya, miji na manispaa huku akiwahamisha vituo wakurugenzi 19, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kujaza nafasi zilizowazi.

Rais Dkt. John Magufuli

Katika mabadiliko hayo, Rais Magufuli pia amembadilisha kituo cha kazi mkuu wa wilaya ya Kwimba, Mhandisi Msafiri Simeoni na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato na kumteua Senyi Simon kuenda kushika nafasi yake.

Akisoma uteuzi huo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amewataka wakurugenzi wote wapya kuripoti siku ya Jumatano, Agosti 15, 2018 katika ofisi za Katibu Mkuu wa TAMISEMI pia watakapokwenda Dodoma wanapaswa kuwa na vyeti vyao vya kidato cha nne, sita na elimu ya taaluma.

"Wakurugenzi ambao katika mabadiliko haya wamebadilishwa vituo vya kazi, wanapaswa kwenda kuripoti katika vituo vyao vya kazi mara moja. Na kwa wale wakurugenzi walioteuliwa kwa mara ya kwanza wanatakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI Agosti 15 mwaka huu kwa ajili ya kiapo cha uadilifu na maelekezo ya majukumu yao", amesema Balozi Kijazi.

Mbali na hilo, Rais Magufuli amemuamisha kituo cha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Kakonko Mkoa wa Kigoma Lusubilo Mwakabili na kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Temeke. Pia amemteua Beatrice Kwai kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Ubungo na Mwilabu Nyabusu amemteua kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Kigamboni.

Uteuzi huo wa Rais Magufuli unakuwa wa pili kufanyika kwa kufanya mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi ambapo wa kwanza ulikuwa ni Julai 28, 2018 ambapo aliteua wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na makatibu tawala.
.