Ijumaa , 2nd Jul , 2021

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa mara ya mwisho kuonana na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale ni mkoani Mwanza kwenye daraja la JPM ambapo alimpa maelezo ya kina jinsi atakavyolijenga na kulikamilisha daraja hilo la Kigogo- Busisi.

Rais Samia na Mhandisi Patrick Mfugale walipokutana kwa mara ya mwisho mkoani Mwanza, kwenye daraja la JPM

Kauli hiyo ameitoa leo Julai 2, 2021, Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa salamu za pole na rambirambi kwa niaba ya serikali wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Mhandisi Mfugale iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee na kusema kuwa kifo chake kimeaacha pengo kubwa kwa familia na Taifa kwa ujumla.

"Mara ya mwisho nimeonana na Mhandisi Mfugale ni pale nilipotembelea daraja la JPM la Kigongo-Busisi, nilimkuta akiwa makini na kunipa maelezo ya kina kuhusu ujenzi wa daraja lile, na matumaini yake jinsi ya kulijenga na kulikamilisha, bahati mbaya Mungu amemchukua kabla matumaini yake kutimia," ameeleza Rais Samia.

Mhandisi Patrick Mfugale, alifariki dunia Juni 29, 2021, katika hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma, alipofikishwa kwa ajili ya matibabu baada ya kuugua ghafla.