Alhamisi , 26th Feb , 2026

Upatikanaji wa samaki jijini Tanga umeendelea kuwa kitendawili, hasa katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo mahitaji ya kitoweo hicho huongezeka kwa kasi, wakati meza nyingi za futari zikitegemea samaki kama chakula kikuu, hali imekuwa tofauti sokoni — samaki ni wachache

Upatikanaji wa samaki jijini Tanga umeendelea kuwa kitendawili, hasa katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo mahitaji ya kitoweo hicho huongezeka kwa kasi, wakati meza nyingi za futari zikitegemea samaki kama chakula kikuu, hali imekuwa tofauti sokoni — samaki ni wachache, bei zinapanda, na matumaini ya wavuvi yanazidi kufifia.

Wavuvi wameiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vya uvuvi ikiwemo boti na meli zenye uwezo wa kufika katika kina kirefu cha bahari, ili waweze kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya wananchi.

Uwekezaji katika uvuvi wa kisasa unaelezwa kuwa suluhisho la kudumu, si tu kwa kuinua kipato cha wavuvi bali pia kuhakikisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa taifa kwa njia endelevu.

Wakizungumzia changamoto ya upungufu wa samaki katika Mwalo wa Deep Sea, baadhi ya wavuvi walisema tatizo kubwa ni samaki kuhamia katika kina kirefu cha maji, huku wao wakilazimika kutumia zana za kizamani zisizoweza kufika mbali zaidi baharini.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi Mkoa wa Tanga, Issa Khatibu, amesema kwa miaka mingi uvuvi mkoani humo umekuwa na tija ndogo kutokana na kufanyika zaidi katika maeneo ya karibu na ufukwe, hali inayopunguza mavuno na kipato cha wavuvi.

Wavuvi hao sasa wanaiomba Serikali pamoja na wadau wa sekta ya uvuvi kushirikiana katika kuboresha miundombinu ya uvuvi na upatikanaji wa zana za kisasa. Wanaamini kuwa hatua hiyo si tu itarejesha wingi wa samaki baharini, bali pia itaimarisha kipato chao na kuhakikisha wananchi wanapata kwa urahisi kitoweo hicho muhimu