Alhamisi , 8th Nov , 2018

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimejitokeza juu ya kushikiliwa kwa waandishi wa habari wawili ambao ni Raia wa kigeni na wanaharakati wa kamati maalum ya kuwalinda wanahabari Duniani CPJ.

Mkurugenzi wa Itifaki na mambo ya nje wa CHADEMA, John Mrema, Mrakibu wa Polisi, Msemaji Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda.

Waandishi hao waliokamatwa ni Mkuu wa kamati ya Afrika, Angela Quintalna Muthoki Mumo ambaye ni mwakilishi wa kamati hiyo ya Afrika mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Itifaki na mambo ya nje wa CHADEMA, John Mrema ameitaka idara ya uhamiaji nchini kurejesha Passport zao ili kuwapa nafasi waandishi hao wa kigeni kufanya kazi kwa uhuru.

"tunaitaka idara ya uamiaji ituambie imetumia sheria gani kuwakamata waandishi hao wa kigeni, pia tunaitaka serikali iseme kwa uwazi nani alitoa amri ya kukamatwa kwa waandishi hawa, na mwisho iboreshe maisha ya kufanyia kazi kwa waandishi wa habari."

Mapema jana ilielezwa kuwa Maafisa waliojitambulisha kuwa wanatoka Idara ya Uhamiaji, waliwakamata viongozi wao katika Hoteli waliyofikia jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Jijini Dar es salaam, Mrakibu wa Polisi, Msemaji Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda amesema waliwashikilia waandishi hao wawili na leo hii wamerejeshewa pasipoti zao.

"Ni kweli tuliwashikilia kwa muda, tulifanya mahojiano nao, tulizikamata paspoti zao na sasa tumewarejeshea. Tumewaelekeza wafuate taratibu lakini tumewakabidhi pasipoti mbele ya ubalozi wao," amesema Ally Mtanda.