Alhamisi , 18th Jul , 2019

Serikali nchini Uganda imedhamiria mpango wa kuwasajili wakulima na ng'ombe wao kwa ajili ya kurahisisha utambuzi na kuwawezesha fursa za soko la Kimataifa.

Ng'ombe

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Vincent Ssempijja alipokuwa akizindua maonesho ya wakulima katika viwanja vya Nile mjini Jinja, ambapo amesema soko la Kimataifa linataka nchi zinazozalisha mazao hayo kusajili.

"Wanahitaji kujua bidhaa wanazonunua zinatoka wapi, wamekuwa wakikataa kulipa na kuzuia bidhaa zilizosafirshwa kutoka Uganda pindi wanakuta boksi moja lina shida", amesema Waziri Ssempijja.

"Wakulima watasajiliwa na bidhaa wanazozalisha zitapewa utambuzi wa 'barcodes', ili kama wakigundua box lina kasoro, wafuatilie chanzo na kurekebisha. Hatuwezi kuingia katika soko la aina hiyo hadi hapo tutakapowasajili".

Pia kuhusiana na suala la usajili wa ng'ombe, Waziri huyo wa Kilimo amesema, "kwa wafugaji wa ng'ombe watasajiliwa wenyewe na ng'ombe wao pia watasajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa kwa sababu walaji wanahitaji nyama ya ng'ombe yenye umri kati ya miezi 15 hadi 24. Kwahiyo tunakwenda kuuza kutokana na umri wao".

Kilimo ni moja ya sekta muhimu katika uchumi wa nchi ya Uganda kwa masuala ya ajira na chakula, huku kikichangia asilimia 25 ya ukuaji wa pato la ndani la taifa (GDP).