Jumamosi , 15th Oct , 2016

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini -TANROADS, imeanzisha Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri -TECU, ili kuwajengea uwezo wahandisi wazawa kusimamia miradi ya ujenzi wa barabara nchini

Moja kati ya miradi ya barabara inayotekelezwa nchini

Akizungumza mkoani Geita mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga-Biharamulo yenye urefu wa Kilometa 112 ambayo pia inasimamiwa na Wahandisi Washauri Wazawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema mpaka sasa wahandisi wazawa wanasimamia miradi mbalimbali ya barabara katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita na Kilimanjaro ambapo kupitia miradi hiyo serikali imeokoa dola za kimerani milioni mbili ambazo zingetumika kulipa wahadisi kutoka nje ya nchi.

Waziri Mbarawa ameongeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa miaka mitano ijayo miradi yote mikubwa nchini itasimamiwa na Wakala huo ili kuokoa fedha za ndani na badala yake fedha hizo kuelekezwa kwenye miradi mingine ya ujenzi.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Geita Mhandisi Harun Senkuku amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Uyovu-Bwanga umefikia asilimia 47 na Bwanga - Biharamulo umefikia asilimia 42 na ujenzi wake unagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 90.

Naye, Mhandisi Msahauri kutoka TECU Gladson Yohana amesema kuwa kusimamia miradi mikubwa kama hiyo kumewasaidia kujifunza zaidi kwa vitendo na amemuhakikishia Waziri huyo kusimamia barabara hiyo kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyotakiwa.