Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Serikali imeombwa kurejesha ruzuku iliyokuwa inawapatia watu walio na ulemavu ili iwasaidie kutekeleza majukumu ya kuendesha vyama vyao,ili waondokane na tatizo la kupita mitaani kuomba.

Ombi hilo limetolewa na mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVIWATA) mkoani Lindi, Mussa Bakari Namulya kwa Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Stella Alex Ikupa, katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo mjini Lindi.

Namulya akiwasilisha ombi hilo, amesema ruzuku waliyokuwa wakipewa na serikali hapo mwanzoni iliweza kuwasaidia katika uendeshaji wa vyama vyao, katika kupanga majukumu mbalimbali ya maendeleo, hivyo kuwapunguzia tatizo la kupita mitaani kuomba misaada kwa jamii.

Naibu waziri huyo Mhe.  Ikupa akizungumza baada ya kusikiliza ombi pamoja na kero zingine zinazowakabiri amehaidi Ofisi yake italifanyia kazi kuona namna ya kuweza kuirejesha huku akiwasihi walemavu wote nchini, kuwa na upendo na ushirikiano mzuri ili kuondoa migongano ya wenyewe kwa wenyewe.