Serikali yatoa maamuzi kuhusu ving'amuzi kuonesha

Jumanne , 14th Mei , 2019

Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Atashasta Nditiye, amesema serikali inashughulikia maombi ya makampuni yanayotaka leseni ya kubeba maudhui ya vituo vya televisheni vya ndani ili yaweze kupata leseni stahiki.

Satelite

Naibu Waziri huyo ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyamagana kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe. Stanslaus Mabula, aliyetaka kujua kama serikali haioni kufungia ving'amuzi vya Azam TV, DSTV na vinginevyo kuonesha vituo vya televisheni vya hapa nchini kuonekana katika vingamuzi hivyo ni kuwanyima raia haki ya kupata  taarifa.

Mhe. Nditiye amesema serikali inatambua umuhimu wa wananchi kupata fursa ya kujua mambo  yanayoendelea kwenye taifa, kwa misingi hiyo imetoa leseni zenye masharti tofauti ikiwemo leseni za utangazaji wa umma ambapo matangazo huruhusiwa kurushwa na watoa huduma wote.

Amesema kwa sasa matangazo ya umma ni TBC 1 na TBC 3 maarufu kama Safari Channels na kuongeza kuwa makampuni yanayomiliki visimbuzi vya  DSTV, ZUKU na AZAM TV, hayakustahili kutoa huduma ya  kubeba vituo vya televisheni vya hapa nchini kutokana na masharti ya leseni zao.