Shamba la bangi lateketezwa Mbeya

Friday , 17th Feb , 2017

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kipolisi Mbalizi lilifanya Oparesheni ya pamoja na kumkamata mkulima mmoja wa dawa za kulevya aina ya bangi, pamoja na kuteketeza shamba lake.

Shamba la bangi pamoja na mafurushi ya bangi yaliyokuwa nyumbani kwa mtuhumiwa

Kamanda wa Polisi Mkioa wa Mbeya DCP Dhahiri Kidavashari amesema tukio hilo limetokea tarehe 16 Februari mwaka huu na kumtaja mtu huyo kuwa ni Upe Nduta mwenye umri wa miaka 30, mkazi wa Jojo Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi, ambaye alikuwa amelima shamba lenye ukubwa wa ekari moja.

Aidha katika Oparesheni hiyo zaidi ya miche 2,000 iliyokomaa ilikutwa shambani kilogram 2 na gram 145 za bangi pia zikikutwa nyumbani kwake.

Kamanda Kidavashari amesema mtu huyo muuzaji/msafirishaji na mtumiaji wa dawa za kulevya .

Katika hatua nyingine, kwa nyakati tofauti, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limekamata watuhumiwa wanne wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi misokoto mitatu yenye uzito wa kilogram 15 na gram 685 kati ya tarehe 11 Febriari hadi 16 Februari, 2017.