Sheikh Ponda ametoa kauli hiyo akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari nchini
"Ningekutana na kiongozi wa juu ningemshauri kuhakikisha kwamba anaweka misingi imara ili tasnia ya habari iepukane na hii hali ya kuwa na sheria ambazo zinapunguza ule uwezo wao wa kufanya kazi tunaweza kusema sheria kandamizi"
"Vyombo vya habari vikiwa huru vitaaminika kwa umma, maana yake vitaeleza au vitawasilisha zile fikra za umma kwa usahihi na vitasaidia sana utawala pamoja na sekta binafsi kwa maana vitasaidia sana kutathmini zile shughuli zao" amesema Sheikh Ponda
Aidha ameongeza kuwa uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari utasaidia kutoa elimu mbalimbali na ambayo inahitajika na jamii na vitaifikisha kwa umma kwa jinsi inavyotakiwa
Akizungumzia uhusiano kati ya vyombo vya habari na uwepo wa Demokrasia Ponda amesema kuwa kama nchi inakuwa na Demokrasia basi vyombo vya habari vinakuwa hai
"Kukiwa kuna Demokrasia vyombo vya habari vinakuwa hai, maana yake sheria zitakuwa nzuri sio zile za ukandamizaji, kwa sababu kinyume cha Demokrasia ni udikteta yani mabavu, watu hawapati uhuru wa kutoa mawazo kuzungumza na kukosoa" amesema Sheikh Ponda Issa Ponda
Aidha kiongozi huyo wa dini amekemea baadhi ya viongozi wa dola wanaosema kuwa huwa hawafanyi kazi zao kwa kuangalia vyombo vya habari vinasemaje na kusema ni vyema vyombo vya habari nchini vikatumika katika ujenzi wa Taifa
"Mara nyingi viongozi wa dola huwa wanatumia kauli kuwa hawafanyi kazi kwa kuzingatia vyombo vya habari, mimi kama ningekutana na kiongozi wa juu ningemshauri kwamba vyombo vya habari visitazamwe hivyo, isipokuwa wavitumie vyombo vya habari katika ujenzi wa Taifa"
