
Hashm Mgandilwa katika katika mahojiano na kipindi cha Super Mix kilichokuwa kikiruka kutoka Kigamboni Dar es Salaam
Mgandilwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kigamboni na kujibu maswali yao papo kwa hapo katika kipindi cha SUPAMIX ambacho leo kimeruka mubashara kutoka wilaya ya Kigamboni.
“Vijana wa bodaboda tafadhali nawaomba na kuwataka kuwa makini na vyombo vyenu, mimi sikuchaguliwa kuwa mkuu wa wilaya wa makaburi, ila nilichaguliwa kuwa mkuu wa wilaya wa watu na nataka kushirikiana na watu katika kiutendaji wa kazi hivyo tambueni thamani ya maisha yenu na kuwa makini barabarani” Amesema Mgandilwa,
Aidha mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi wote ambao wanazingirwa na maeneo ya jeshi na ambao wameshapewa taarifa juu ya kuwepo kwenye eneo la jeshi wasubiri hadi watakapolipwa fidia ili waweze kuondoka kwa amani.
Pamoja na hayo Mgandilwa amewataka wananchi kushirikiana kikamilifu katika zoezi la usafi katika maeneo yao ili kujiepusha na magonjwa yanayoepukika.
Wakati huo huo mkuu huyo wa wilaya amewatoa hofu wananchi wake kwamba pamoja na kwamba wilaya hiyo ni mpya serikali imejipanga vyema katika kuhakikisha huduma za afya, maji, usafiri zinaimarishwa ili kuendana na kasi ya maendeleo.
