Jumamosi , 5th Dec , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, ametangaza Mawaziri 21 wa Wizara mbalimbali aliowateua na kutangaza Manaibu Mawaziri 23, na kati ya hao yumo David Silinde aliyekuwa CHADEMA na kisha kuhamia CCM, yupo pia aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi.

Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, mteule, Patrobas Katambi na kulia ni Naibu Waziri TAMISEMI David Silinde.

Baraza hilo limetangazwa hii leo Desemba 5, 2020, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Ikulu ya Chamwino Dodoma, ambapo mbali na kutangaza mawaziri, Rais Magufuli pia ameongeza Wizara mpya ambayo ni Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambayo Waziri wake ni Dkt. Faustine Ndugulile.

"Wizara ya ulinzi aliyeteuliwa kuwa waziri ni Elias Kwandikwa, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, aliyeteuliwa kuwa Waziri ni Capt. George Mkuchika, Wizara ya Ardhi ni William Lukuvi, Wizara ya Maji ni Jumaa Aweso, Wizara ya Habari ni Innocent Bashungwa", ametangaza Balozi Kijazi.

Aidha wengine ni "Wizara ya Mifugo na Uvuvi aliyeteuliwa kuwa Waziri ni Mashimba Ndaki, Waziri wa Kilimo ni Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Viwanda na Biashara Goeffrey Mwambe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ni Ummy Mwalimu, Patrobas Katambi kateuliwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira".

"Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ni Mwita Waitara, Naibu Waziri TAMISEMI ni David Silinde", ametangaza Balozi John Kijazi