Alhamisi , 16th Mei , 2019

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa amemuandikia barua Rais wa Bunge la Afrika ili kusitisha uwakilishi wa Stephen Masele katika bunge hilo kutoka Tanzania ambaye pia ni makamo wa Rais.

Spika Ndugai.

Spika amesema hayo leo Mei 16, 2019 bungeni wakati akitoa taarifa mbele ya bunge ambapo amefunguka kuwa wamemsimamisha kutokana na utomvu wa kinidhamu na kulidhalilisha taifa.

"Nimemuandikia barua Rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi wake, hadi Kamati ya Maadili itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, na hapa kuna kamati mbili zinamsubiri ikiwemo Kamati ya Maadili ya Bunge na Kamati ya Maadili ya chama chake", amesema Ndugai.

Ndugai ameongeza kuwa, "Stephen Masele ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyohovyo, ndiyo maana tumemuita atufafanulie huenda yuko sahihi, lakini anafanya mambo ambayo ni hatari kubwa, amekuwa akichonganisha mihimili miwili, ni amejisahau sana".

Stephen Masele Makamo wa Rais Bunge la Afrika.

Mbunge huyo wa Shinyanga mjini (CCM) alichaguliwa kuwa makamo wa Rais wa Bunge la Muungano wa Afrika (PAP) Mei 10, 2018.