Jumapili , 14th Apr , 2019

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kitendo cha Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Assad kuendelea kuwepo ofisini mpaka sasa ni kumpa rais wakati mgumu kwa kuwa wao bunge wameshaeleza kuwa hawamtaki.

CAG Prof. Mussa Assad, Spika Job Ndugai

Ndugai ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanahabaji Jijini Dodoma ambapo amesema kwamba kwa kitendo cha Bunge kumkataa Prof Assad alipaswa ajiongeze kwa kujiuzulu ama la!

"Tunataka tumuoneshe Prof. Assad kuwa Bunge halichezewi, simuelekezi kazi  ila anatakiwa ajiongeze kama ni kujiuzulu au la! maana tushamwambia  hatumtaki, anavyoendelea kubaki ofisini ni kumpa tu wakati mgumu Rais"

https://twitter.com/eastafricatv/status/1117373181092880384

"Sisi kama Bunge hatutaki hilo neno dhaifu, kwa sababu Bunge kama Bunge  halifanyiwi tathmini na ofisi ya CAG ila wanaofanyiwa tathmini ni  watendaji wa Ofisi hiyo hivyo hawakupaswa kudhihakiwa na lugha hiyo  inayotajwa kuwa ya kihasibu".

Aidha kuonyeshwa kukerwa na neno 'Dhaifu analoendelea kulitumia Prof Assad, Ndugai amesema kwamba  kama yeye analipenda sana neno hilo ajiite na kwamba wao kama bunge wameikataa na hawalipendi.

Kuhusu kazi za CAG, Spika amefafanua kwamba "Hatuna tatizo na ripoti ya CAG…tatizo letu ni maneno ambayo Prof. Assad ameyatoa akiwa Marekani, na alipoita waandishi akarudia  tena, maneno yale sie tumeyakataa sio ya kistaarabu".