Spika awataka Wabunge wakae 'miaka 45' Bungeni

Jumatatu , 9th Sep , 2019

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, amemualika Bungeni Mbunge aliyekaa kwa muda mrefu jimboni kwa miaka 45, Chrisant Majiyatanga Mzindakaya na kuwataka Wabunge wote waige mfano wake.

Kwa mujibu wa Ndugai amemuita Mbunge huyo wa zamani kutoka Mkoa wa Rukwa ili awe funzo kwa Wabunge vijana, huku akikiri kwa sasa hakuna Mbunge anayeweza kukaa kwenye Ubunge kwa miaka mingi.

"Leo nimemualika maalum hasa kwa Wabunge vijana muweze kumfahamu huyu alikuwa Mbunge kwa miaka 45 mfululizo, hii ni rekodi ambayo hamuwezi kuifikia hata mtambike, alianza 1945 hadi 2010." amesema Ndugai.

"Mzindakaya amepata tuzo mbalimbali za utumishi ikiwemo tuzo ya Mwalimu Nyerere, tuzo kutoka Umoja wa Vijana, aliandikiwa barua na Rais Mwinyi ya kupongezwa kwa utendaji kazi wake, naomba mfuate nyayo zake" amesema Spika Ndugai.

Kwa sasa Bunge linaendelea jijini Dodoma ambapo Wabunge wanajadili miswada mbalimbali kabla ya kupitishwa kuwa sheria.