Ijumaa , 15th Apr , 2016

Rais Magufuli na Rais Salva Kiir wasaini mkataba wa kuiwezesha Sudan Kusini kuwa mwanachama kamili wa EAC

Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja na Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini wamesaini Mkataba wa kuiwezesha Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Tukio hilo la kihistoria limefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 15 Aprili, 2016.

Akizungumza wakati wa haflya hiyo, Mhe. Dkt. Magufuli aliipongeza nchi hiyo na kusema kuwa anajivunia tukio hili la kihistoria kutokea wakati Tanzania ikiwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba ukurasa mpya wa ushirikiano na mahusiano na nchi hiyo umefunguliwa.

Aliongeza kuwa kihistoria Sudan Kusini, imekuwa na mahusiano ya karibu na nchi za Afrika Mashariki katika nyanja mbalimbali ikiwemo mwingiliano wa tamaduni, ushirikiano wa kibiashara na uchumi na ukaribu wa kijografia. Aidha, alieleza kuwa kujiunga kwa Sudan Kusini kwenye EAC kunaifanya Jumuiya hii kuwa na soko kubwa lenye takriban watu milioni 160.

Vile vile Mhe. Rais Magufuli alisema kuwa ili Jumuiya ya Afrika Mashariki iweze kuwa na maendeleo endelevu suala la kudumisha amani ni la msingi, hivyo aliwahimiza Sudan Kusini kuendeleza juhudi kwenye mazungumzo ya amani.

‘’Dhana ya Mtangamano ni kukuza biashara, uwekezaji na miundombinu ili kujiletea maendeleo endelevu katika Jumuiya yetu, hivyo nahimiza umuhimu wa nchi wanachama kudumisha amani ili kufikia malengo tuliyojiwekea ‘’ alisema Rais Magufuli.

Wakati huohuo, Rais Magufuli alimpongeza Rais Kiir kwa jitihada zake katika kuhakikisha nchi yake inajiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki haraka ambapo miezi minne baada ya nchi hiyo kupata uhuru iliwasilisha maombi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na miaka mitano imeweza kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Rais Kiir alieleza kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa na nchi yake ya kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, alimshukuru Rais Magufuli na Marais wa Nchi zote wanachama kwa kuiunga mkono nchi yake kwa kauli moja.

Mhe. Kiir aliongeza kuwa uamuzi wa nchi yake wa kujiunga na Jumuiya ni wa dhati na kwamba una nia ya kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa ujumla, ambapo nchi yake imeshaanza kufanyia mabadiliko mifumo mbalimbali kwenye Serikali yake ili kuweza kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za mtangamano ikiwemo kuunda Wizara inayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

‘’Hatimaye Sudan Kusini imerudi nyumbani. Jumuiya ya Afrika Mashariki ni sehemu sahihi kwa nchi yangu kwani Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mtangamano unaoheshimika Afrika na Duniani kwa ujumla’’ alisisitiza Rais Kiir.

Pia, Rais Kiir alitangaza kufunguliwa rasmi kwa Ubalozi wa nchi yake hapa nchini na tayari amemteua Balozi Mariano Deng Ngor kuwa Balozi wa Sudan Kusini nchini Tanzania.

Awali akizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha wananchi wa Sudan Kusini waliothirika na migogoro na kuikimbia nchi yao wanarejea kwa ajili ya kuendeleza nchi yao.

Jamhuri ya Sudan Kusini ilipata uhuru wake tarehe 09 Julai, 2011 na iliwasilisha maombi rasmi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 10 Novemba, 2011. Aidha, Tangazo la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha mwezi Machi 2016.