Jumatano , 3rd Jun , 2015

Uhusiano baina ya Tanzania na Finland ni wa kudumu na utaimarishwa na kutafutiwa namna ya kuukuza zaidi ya hapa ulipo sasa.

Rais Sauli Niinisto wa Finland amemueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 2 Juni, Ikulu, jijini Helsinki wakati wa Mazungumzo baina ya viongozi hao.

"Uhusiano wetu ni wa muda mrefu, ni uhusiano ambao umedumu kwa miaka 50, tumekuwa na uhusiano ambao umeleta maendeleo ya kiuchumi kwa Tanzania". Rais Niinisto amesema, na kuongeza kuwa, "Hii inatupa nafasi ya kutafuta mbinu mpya za kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano huu zaidi".

Rais Kikwete aliwasili Helsinki tarehe 1 Juni,2015 kwa ziara ya kikazi ya siku 3 ambapo pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Niinisto kwa mwaliko wake ambapo amemuelezea hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

Rais pia amemueleza mwenyeji wake kuhusu uchaguzi mkuu ujao nchini Tanzania na kuweka bayana kuwa, "Nimekuja kukushukuru pamoja na wananchi wa Finland kwa ujumla kwa mchango na misaada yenu ya maendeleo kwa Tanzania tangu nchi yetu ipate uhuru hadi leo na bado uhusiano wetu upo imara".

Rais Kikwete amesema na kuomba Finland kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuletea watu wake maendeleo. Rais Kikwete pia anatumia ziara hii kuwaaga na kuwashukuru viongozi na washirika wa Tanzania katika maendeleo, ambao wametoa mchango mkubwa na msaada kwa serikali na wananchi wa Tanzania katika kipindi chake cha uongozi.

Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Wabunge wa Finland ambao ni viongozi wa vyama vya siasa nchini humo, wakiongozwa na Spika wao Bi. Maria Lohela. Bi. Lohela amesema, Rais Kikwete ndiye kiongozi mkubwa wa nje kutembelea na kufanya mazungumzo na Wabunge hao ambao wameshika nyadhifa zao mpya kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.

Rais Kikwete amemueleza Spika Lohela kuhusu kuisha kwa muhula wa Bunge la sasa nchini Tanzania ambapo, Spika Lohela amesema bunge la Finland linapenda kuendeleza ushirikiano na Bunge la Tanzania na hivyo kutoa mwaliko kwa wabunge wapya watakaochaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.

Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, ametembelea chuo Kikuu cha Aalto jijini Helsinki ambacho ni chuo cha 3 kwa ukubwa nchini Finland. Chuo cha Aalto kina utaratibu wa kubadilishana wanafunzi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Rais Kikwete anatarajia kumaliza ziara nchini Finland tarehe 3 Juni,2015 kwa kukutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa sekta mbalimbali kabla ya kuelekea nchini Sweden kuendelea na ziara yake ya kikazi kufuatia mwaliko kutoka kwa Waziri Mkuu wa Sweden Bwana Stefan Lofven.

Imetolewa na;

Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Helsinki - Finland
3 Juni, 2015