Alhamisi , 27th Oct , 2022

Serikali ya Jamhuri ya Korea imeipatia Tanzania mkopo wa gharama nafuu wa shilingi bilioni 310 kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri Mkuu wa Korea Han Duck – Soo wakishuhudia zoezi la utiaji saini

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo baina ya Serikali ya Tanza na Korea Kusini itakayotolewa kupitia benki ya Exim ya Korea, imefanyika leo Oktoba 27, 2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Korea Kusini iliyopo Seoul.

Mkataba wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA una thamani ya shilingi bilioni 161 na mkataba wa uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi ambao una thamani ya shilingi bilioni 149.

Akizungumza wakati wa halfa hiyo ambayo ambayo pia ilishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Korea Han Duck-Soo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania na Korea zinajivunia mahusiano yaliyodumu kwa miaka 30 ambayo yamekuwa chachu katika kukuza uchumi wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.

“Tunaishukuru sana Korea Kusini kwa kuwa miongoni mwa mataifa yanayoshiriki katika kutatua changamoto za kimaendeleo ikiwemo kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF)” amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Majaliwa amesema kuwa kupitia mfuko huo, Tanzania imeweza kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo madaraja, barabara, kituo cha kisasa cha kusajili meli cha Zanzibar, njia ya kusafirishia umeme, hospitali ya Mloganzila, mradi wa umwagiliaji uliopo Zanzibar na utoaji huduma wa vitambilisho vya Taifa.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Tanzania Nchini Korea Kusini, Balozi Togolani Mavura, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi na watendaji wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.